Tafadhali Tuunge Mkono
|
CHADEMA kinaamini kwamba ili uongozi wa nchi uweze kuzingatia maslahi ya Watanzania kwa umakini na kwa dhati hatuna budi tuwe na siasa za ushindani thabiti. Yaani Bunge lenye wapinzani wa kutosha ambao ni wazalendo makini na jasiri, wenye uwezo wa kuikosoa Serikali bila woga pale inapozembea. Hali kadhalika mfumo wa serikali za wilaya, vijiji na mitaa ni laizma uwe na mazingira yanayowezesha kukosoana na kusahihishana kwa uhuru na uwazi bila woga ili kuondoa au kuzuia ubadhirifu wa mali ya umma, uzembe, uonevu, rushwa na papo hapo kuhakikisha tunakuwa na maendeleo ya kudumu na ya kuridhisha.
CHADEMA inadhamiria kuhamasisha na kutoa elimu ya uraia mwema na elimu ya siasa kwa Tanzania nzima katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa 2009. Tunatarajia wazalendo wenye uchungu na nchi yao na wenye dhamira ya dhati ya kutatua matatizo sugu ya nchi hii, kuungana nasi katika juhudi hii. Uongozi wa CHADEMA unataka kujadili na wananchi, wakichangia mawazo yao kwa uhuru na uwazi. Kila kijiji, kitongoji au kata pawepo na sera na mikakati iliyobuniwa na wakazi wake inayolenga kuondoa kero zinazowakabili jamii husika.
Ili kuwezesha uongozi wa CHADEMA katika ngazi zote - kuanzia tawi la kitongoji hadi taifa - uweze kutekeleza majukumu haya ya uenezi na uhamasishaji lazima pawepo nyenzo na vifaa. Kwa hiyo tunakaribisha Mtanzania yeyote mwenye kupenda nchi yake, na anayeamini katika ujumbe huu atoe mchango kadri ya uwezo wake. Naam, kimefika kipindi cha Watanzania wema kutusaidia.
Wasamaria wema wametuchangia fedha, wengine wametoa sehemu za nyumba zao kama ofisi ya matawi ya chama. Wengine wamewakarimu viongozi au kuwapa malazi huko vijijini. Wengine wametukodishia kwa gharama nafuu magari yao au kutupa petroli bure tuweze kutembelea wilaya zao. Wengine wametupatia baiskeli tuweze kuwafikia sehemu ambazo magari hayafiki. Wako waliotuazima vipaza sauti tuweze kuhutubia mikutano yetu ya hadhara. Vilevile wengine wamehudhuria na kushangilia na kuwapa moyo wale waliowaeleza misimamo ya CHADEMA. Wote hao wamechangia na tunaomba waendelee mpaka hapo lengo letu litakapofikiwa. Tunawasifu, tunawashukuru sana na mungu awazidishie.
Kama hutaweza kufika kwenye ofisi za CHADEMA basi tuma fedha katika akaunti zetu zifuatazo:
Akaunti ya "CHADEMA"
NBC Corporate Branch (Local currency) 011103010075
NBC Samora Branch (Foreign currency) 012105019310
au
Akaunti ya "Freeman A. Mbowe and W.P. Slaa"
NBC Corporate Branch (Local currency) 011101016268
NBC Corporate Branch (Foreign currency) 011105010534
Jambo muhimiu na la lazima ni kwamba ili kufanikisha lengo letu la kuimarisha utawala bora na maendeleo endelevu ya kuridhisha, hatuna budi kudumisha misaada hii. MwanaCHADEMA hakikisha kadi yako unailipia ada ya mwaka, na kama una uwezo changia tawi lako ili CHADEMA kiweze kununua makaratasi na mabango ya uenezi. Wewe mzalendo mwenye uwezo zaidi tupe mchango wa kweli utakaodhihirisha mapenzi yako kwa chama. Kila fedha itakayopokelewa CHADEMA itaambatana na stakabadhi yenye jina la mtoaji au jina la 'kificho' kama mtoaji atapendelea. Tunaelewa na tunaheshimu sababu zao wale wote wasiotaka majina yao yahusishwe na CHADEMA hadharani.
Hivyo ndivyo kuchangia kwa hali na mali. Tunaamini na kudhihirisha kwamba hii ndiyo nguvu ya Umma.
Changia CHADEMA! Changia Maendeleo endelevu!
Asanteni sana
Dk. Willibrod P. Slaa
Katibu Mkuu