menuA_3
MWANZO CHAMA SERA KATIBA TUUNGE MKONO UCHAGUZI TUWASILIANE
banner
Mabaraza
»Wanawake
»Vijana
»Wazee
b.part
MengineyoA_3
Mengineyo
»Matamko ya Chama
»CHADEMA Bungeni
»Habari Mpya
»Hotuba mbalimbali
»Makala mbalimbali
»Picha za matukio
»Maoni Yenu
»Katuni

Tamko la Vijana na Wanawake wa CHADEMA juu ya Changamoto zinzokabili Taifa letu

1.0 UTANGULIZI

Sisi wawakilishi wa Baraza la Vijana la CHADEMA (BAVICHA) na wawakilishi wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA) zaidi ya 100 kutoka katika mikoa na wilaya mbalimbali za nchi yetu, tuliokutana katika Semina ya Ujenzi wa Chama chetu iliyofanyika tarehe 1 hadi tarehe 3 June katika ukumbi wa Rombo Green View Hotel jijini Dar es Salaam tunatoa tamko maalum kwa umma wa Watanzania wenzetu na serikali juu ya masuala mazito yanayoendelea kulikabili taifa letu. Tunafanya hivi tukijua kuwa sisi kama sehemu ya chama cha siasa – CHADEMA, tuna haki na wajibu wa kutathmini hali halisi ya taifa letu na kutoa fikra mbadala za kuondoa mapungufu yaliyopo katika utendaji wa serikali yetu ili kuchochea mustakabali sahihi wa taifa letu. Tunatumia haki na wajibu wetu wa kikatiba, kubainisha mapungufu na kutoa ushauri kwa serikali, kwa vijana wenzetu, na akina mama wenzetu juu ya masuala yafuatayo,

2.0 MASUALA YA KITAIFA

2.1 UFISADI

Tunalaani vikali propaganda zinazofanywa na Waziri Mkuu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kurubuni na kulaghai wananchi kuwa ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi na wanachama wa chama hicho si ufisadi wa CCM. Wataalamu wote wa siasa duniani wanaelezea maana ya chama cha siasa kuwa “Ni kikundi cha watu wenye nia moja, mitazamo na itikadi moja, wakiwa na lengo kuu la kuchukua madaraka ya kuongoza dola”. Kwa mantiki hii chama ni watu, ufisadi wa viongozi wa CCM ni ufisadi wa CCM pia na hasa ikizingatiwa kuwa viongozi hao ndio walipaswa kukiongoza chama hicho katika maadili mema lakini badala yake wamekuwa mstari wa mbele kutenda ufisadi, kutetea ufisadi na kukumbatia mafisadi.

Sisi vijana na wanawake wa CHADEMA tunakubaliana na usemi kuwa “Matendo yana kauli zaidi kuliko maneno”, matendo ya kifisadi yanayofanywa na viongozi wa CCM ndiyo yanayotoa picha halisi kuwa CCM ni chama cha mafisadi kuliko maneno yao ya upotoshaji kuwa chama hicho si cha kifisadi. Kwa hiyo, tunakitaka Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukiri kuwa ni chama cha kifisadi – kwa kufanya hivyo kitajenga imani kwa wananchi kwamba kiko tayari kujisafisha.

Tunakitaka chama chetu – Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kutangaza orodha mpya ya mafisadi mapema iwezekanavyo tukitambua kuwa kuna ufisadi mkubwa uliofanywa na unaoendelea kufanywa ndani ya mashirika, taasisi za umma na idara nyingi za serikali. Orodha mpya ya majina ya mafisadi iongeze wajibu wa Kampeni ya Kupambana na Ufisadi ya chama chetu kushinikiza kuchukuliwa hatua kwa mafisadi hao kama tulivyofanya kwa mafanikio baada ya kutajwa kwa kikosi cha kwanza cha mafisadi kumi na moja (11) mwaka jana.

Tunautaka umma wa watanzania kutuunga mkono na kutuongezea nguvu katika kampeni ya kupambana na mafisadi iliyoanzishwa na chama hiki tangu wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 ili tuisaidie vyema serikali katika kunusuru fedha na raslimali zinazoibwa za taifa letu kwa mustakabali mwema wa vizazi vya leo na vijavyo. Ikumbukwe kuwa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 CHADEMA, kwa nia njema kabisa, tulitoa ujumbe kwa Watanzania kuwa “Tanzania yenye neema haiwezi kuletwa na mafisadi walewale, wa chama kilekile, wakiendeleza uoza ule ule eti kwa Kasi, Nguvu na Ari Mpya. Kwa falsafa ya Chukua Chako Mapema (CCM) Tanzania yenye neema haitawezekana”. Hata baada ya uchaguzi, pamoja na kutofanikiwa kuongoza dola, bado CHADEMA, tuliendelea kusimamia ajenda hii ya kupambana na ufisadi na tukaanzisha kampeni ya kupambana na mafisadi kwa kutumia viongozi wa juu na wabunge wa chama chetu. Ni dhahiri kuwa Kampeni hii ambayo bado inaendelea mafanikio yake tayari yameshaanza kuonekana.Kutokana na kampeni hii, mtuhumiwa wa kwanza katika orodha ya mafisadi iliyotajwa na chama hiki ambaye alikuwa gavana wa Benki Kuu ya Tanzania BOT marehemu Daudi Balali alifukuzwa kazi. Mpaka sasa mawaziri watatu (3) waliotajwa katika orodha ya mafisadi wamelazimika kujiuzulu kwa sababu za kifisadi, hawa ni aliyekuwa Waziri Mkuu Mhe. Edward Lowasa, aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Mhe. Nazir Karamagi, na aliyekuwa Waziri wa Miundombinu Mhe. Andrew Chenge. Kutokana na kampeni hii Raisi alilazimika kuvunja Baraza lote la mawaziri na kuteua mawaziri wapya na kuacha baadhi ya mawaziri waliotajwa katika orodha yetu ya mafisadi akiwemo aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Basil Pesambili Mramba.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio makubwa ya kampeni hii ya kupambana na mafisadi iliyoungwa mkono na wadau mbalimbali vikiwemo vyombo vya habari, bado kazi ya kumaliza ufisadi ni kubwa. Watuhumiwa wa ufisadi wanapaswa kuchukuliwa hatua kali zaidi za kinidhamu na kisheria zaidi ya kufukuzwa kazi na kujiuzulu. Aidha, bado kuna idadi kubwa ya mafisadi ambao hawajachukuliwa hatua hata kidogo, hususani wale wanaohusika na kashfa ya EPA, Benki Kuu, na Richmond.Kwa hiyo, tunaitaka serikali kuwasilisha Bungeni ripoti ya EPA haraka iwezekanavyo na iwasilishe mapendekezo ya kushughulikia utekelezaji wa Ripoti ya Richmond mara tu baada ya kazi hiyo kukamilika.

2.2 KUPANDA KWA BEI YA CHAKULA

Sisi vijana na wanawake wa CHADEMA, tunatambua kuwa nchi yetu pamoja na nchi nyingi duniani, hivi sasa inakabiliwa na tatizo la kupanda kwa bei za vyakula kufuatia kupanda kwa bei ya mafuta duniani. Tatizo hili limeshaanza kuwaathiri wananchi wengi maskini kwa kushindwa kumudu gharama za vyakula na pia limesababisha serikali kuanza kufunga shule za bweni kwa sababu za ukosefu wa chakula. Tatizo limeanza kuwa kali zaidi ndani ya nchi yetu kutokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu taifa letu limeshindwa kujitosheleza kwa chakula kwa sababu ya kutokuwepo sera makini za kuboresha kilimo na kutokuwepo jitihada za dhati za kukuza uzalishaji mkubwa wa mazao ya chakula. Kwa hiyo, tunakitaka kikao cha Bunge la Bajeti kinachoanza leo, kulijadili kwa makini suala hili na kupitisha bajeti ya kutosha itakayowezesha serikali kuagiza chakula cha kutosha na kuhifadhi kilichopo ili kunusuru uhai wa watanzania wengi maskini. Kihakikishe kuwa kinapunguza kodi ya uingizaji wa mafuta nchini, na kikao hicho kipitishe bajeti ya kutosha ya kuchochea maendeleo ya kilimo.

Sisi vijana na wanawake wa CHADEMA tunaamini kuwa ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ukosefu au upungufu wa chakula katika nchi hii, utapatikana kwa kuwa na sera makini na zinazotekelezeka za kilimo cha uzalishaji mkubwa na zitakazowezesha kuhifadhiwa kwa chakula cha kutosha pamoja na kuwa na viongozi wenye nia ya dhati ya kuendeleza kilimo badala ya kukifanya kilimo kuwa ni ajenda ya kisiasa tu. Kwa hiyo, tunausihi umma wa watanzania kutafuta ufumbuzi wa muda mrefu kuhusu suala hili kwa kuunga mkono sera mbadala ya CHADEMA kuhusu kilimo na chakula.

3.0 MASUALA YANAYOGUSA WANAWAKE

3.1 UWAKILISHI

Sisi wanawake wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA), tunaunga mkono nia na harakati za kukuza uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya kupitisha sera na maamuzi yaani Bungeni na kwenye Mabaraza ya Halmashauri. Hata hivyo, tunaitaka serikali kuhakikisha mabadiliko yoyote ya mfumo wa uchaguzi yatakayofanywa kwa lengo la kuongeza nafasi za uwakilishi kwa wanawake kwenye vyombo vya kupitisha sera na maamuzi ni vyema yakazingatia misingi ya demokrasia na dhana ya kupata wawakilishi bora wa wananchi badala jambo hili kutekelezwa kwa sifa na manufaa ya kisiasa tu ya chama fulani.

3.2 UJENZI WA SHULE NA ZAHANATI

Tunailaani serikali kwa kutekeleza mkakati haramu wa kuwashinikiza wananchi kuchangia ujenzi wa shule za kata tukijua kuwa huu ni wajibu wa serikali kwa kuwa inakusanya kodi kubwa kutoka kwa wananchi ambayo kama ingesimamiwa vyema ingewezesha kabisa serikali kutimiza wajibu wake kujenga shule bila kuendelea kuwatesa watanzania maskini. Aidha, tunailaani vikali serikali kwa kutopeleka walimu na vifaa vya kutosha katika shule hizo, licha ya wananchi kushinikizwa kuchangia ujenzi wa majengo ya shule hizo.

Tunaionya serikali kutokimbilia kujenga majengo mengi ya zahanati kwa kutafuta sifa za kisiasa tu ilhali bado kuna zahanati nyingi ambazo hazina madawa, vifaa, waganga wala wauguzi. Badala yake, tunaishauri serikali kuongeza kwanza ubora na upatikanaji wa huduma za afya katika zahanati zilizopo kabla ya kuanza kuongeza zahanati nyingine. Tabia hii ya serikali kujenga majengo mengi ya shule na vituo vya afya visivyokuwa vitendea kazi wala huduma, kwa ajili tu ya kutafuta sifa za kisiasa kwa chama kilichopo madarakani CCM, ni dhahiri kuwa haitaleta maisha bora kwa kila mtanzania bali italeta maghofu na maangamizi kwa taifa.

4.0 MASUALA YA VIJANA

4.1 AJIRA KWA VIJANA

Sisi vijana na wanawake wa CHADEMA tunakikumbusha Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali kuhakikisha ahadi ya ajira kwa vijana na maisha bora kwa kila mtanzania zinatimizwa kabla ya uchaguzi mkuu wa 2010. Hadi sasa, hali ya vijana wa kitanzania imekuwa ngumu zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2005.

4.2 UANZISHAJI WA BARAZA LA TAIFA LA VIJANA

Tunatambua kuwa Sera ya Maendeleo ya Vijana toleo la mwaka 2007 inatamka kuwa kutaundwa baraza la taifa la vijana litakalokuwa chombo cha kuwakilisha matakwa na maslahi ya vijana wote bila kujali itikadi za siasa. Tunasikitika kubaini kuwa serikali imeanza mchakato wa siri wa kuunda baraza hili kiserikali, kisirisiri na kiupendeleo kwa kufanya maamuzi ya msingi kuhusu mchakato wa kuunda wa baraza hili bila kuzingatia ridhaa ya vijana wenyewe. Tunawashauri vijana wa kitanzania kuunganisha nguvu katika kudai uhanzishwaji wa baraza huru la vijana litakalofanya kazi kwa maslahi ya vijana badala ya kuwajibika kwa maslahi ya viongozi wa serikali.

Tamko hili limetolewa na washiriki katika Mkutano wa Ndani wa CHADEMA jioni ya Juni 3 na kusambazwa kwa umma leo tarehe 9 Juni, 2008 na:

Mama Mary Jumbe, Afisa Mwandamizi (Wanawake)
Na Dada Regia Mtema, Afisa Mwandamizi (Vijana)

 

lf.curl lf.curl2 rt.curl2 rt.curl
footA_1